KUELEKEA AFCON 2027: MAKUMBUSHO YA TAIFA YAPOKEA MENEJIMENTI YA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KATIKA ZIARA YA KUIMARISHA VIVUTIO VYA URITHI
Makumbusho ya Taifa la Tanzania (NMT) imepokea Menejimenti ya Wizara ya Maliasili na Utalii katika ziara maalum ya kutembelea maeneo mbalimbali ya urithi wa taifa jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Tanzania kuelekea Fainali za Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).
Ziara hiyo imelenga kutathmini hali ya vivutio vya urithi wa taifa na kubaini fursa za kuviboresha, kuviendeleza na kuvitangaza ili viweze kutoa uzoefu bora kwa watalii wa ndani na nje ya nchi watakaotembelea Tanzania wakati wa AFCON 2027. Tanzania itaandaa michuano hiyo kwa ushirikiano na Kenya na Uganda, jambo linalotarajiwa kuongeza idadi ya wageni na watalii nchini.
Menejimenti ya Wizara ilipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Dkt. Noel Biseko Lwoga, akishirikiana na Menejimenti ya NMT, ambapo walifanya ziara katika maeneo mbalimbali yenye historia na urithi mkubwa wa taifa kwa lengo la kujionea hali ya miundombinu, huduma zinazotolewa na fursa zilizopo za kuboresha uzoefu wa wageni.
Maeneo yaliyotembelewa ni pamoja na Makumbusho ya Taifa, Makumbusho ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Nyumba ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyopo Magomeni, Jengo la Old Boma pamoja na Kituo cha Urithi wa Ukombozi Kusini mwa Afrika.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii za kuhakikisha maeneo ya urithi wa taifa yanaandaliwa kwa viwango vinavyokidhi matarajio ya wageni wa kimataifa, huku yakichangia kutangaza historia, utamaduni na utambulisho wa Tanzania.
Makumbusho ya Taifa la Tanzania inaendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na taasisi zake katika kuhifadhi, kuendeleza na kutangaza urithi wa taifa, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kutumia AFCON 2027 kama fursa ya kukuza utalii wa urithi, kuongeza idadi ya watalii na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.

