Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Makumbusho ya Taifa la Tanzania

NAIBU WAZIRI APONGEZA MAKUMBUSHO YA TAIFA KWA MIKAKATI YA KUKUZA UTALII WA URITHI NCHINI

Imewekwa: 16 Jul, 2026
NAIBU WAZIRI APONGEZA MAKUMBUSHO YA TAIFA KWA MIKAKATI YA KUKUZA UTALII WA URITHI NCHINI

Dar es Salaam, Julai 15, 2026 – Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), ameipongeza Makumbusho ya Taifa la Tanzania kwa utekelezaji wa mikakati madhubuti ya kuhifadhi, kuendeleza na kutangaza urithi wa taifa, akisema juhudi hizo zinaendelea kuimarisha utalii wa urithi na kuchangia maendeleo ya sekta ya utalii nchini.

Pongezi hizo amezitoa leo alipofanya ziara katika Makao Makuu ya Makumbusho ya Taifa pamoja na Kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam, ambapo alikagua maendeleo ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za uhifadhi wa urithi wa taifa na maandalizi yanayoendelea ya kuboresha vivutio vya utalii kuelekea Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Chande alisema Serikali inaendelea kuthamini mchango wa Makumbusho ya Taifa katika kulinda historia, tamaduni na utambulisho wa Taifa, huku akisisitiza kuwa urithi wa kitamaduni ni rasilimali muhimu inayoweza kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la utalii duniani.

"Jitihada zinazofanywa na Makumbusho ya Taifa zina mchango mkubwa katika kukuza utalii wa urithi nchini. Ni muhimu kuendelea kuboresha huduma na miundombinu ili wageni watakaofika nchini, hususan wakati wa AFCON 2027, wapate huduma bora na uzoefu wa kipekee wa historia na utamaduni wa Tanzania," alisema Mhe. Chande.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri alipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Dkt. Noel Biseko Lwoga, ambaye aliwasilisha taarifa kuhusu mikakati mbalimbali inayotekelezwa na taasisi hiyo kwa lengo la kuimarisha uhifadhi wa urithi wa taifa na kuongeza mchango wa sekta ya makumbusho katika maendeleo ya uchumi.

Dkt. Lwoga alieleza kuwa taasisi inaendelea kutekeleza maboresho katika miundombinu ya makumbusho, matumizi ya teknolojia za kidijitali katika maonesho, uhifadhi wa malikale na urithi wa kihistoria, pamoja na kuboresha huduma kwa wageni ili kuongeza ubora wa uzoefu wa watalii wa ndani na nje ya nchi.

Aidha, alibainisha kuwa Makumbusho ya Taifa inaendelea kutekeleza maandalizi mbalimbali ya kupokea wageni wanaotarajiwa kuwasili nchini wakati wa AFCON 2027 kwa kuimarisha maonesho, kuboresha mazingira ya kutembelea makumbusho na kuandaa bidhaa na huduma zitakazochochea utalii wa utamaduni na urithi.

Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Chande alitembelea maonesho mbalimbali yaliyopo Kijiji cha Makumbusho, ikiwemo nyumba za asili za makabila mbalimbali ya Tanzania, ambapo alipata maelezo kuhusu historia, mila, desturi na tamaduni zinazoakisi utajiri wa urithi wa taifa na mchango wake katika kujenga utambulisho wa Watanzania.

Akihitimisha ziara yake, Naibu Waziri aliielekeza Menejimenti ya Makumbusho ya Taifa kuendelea kuimarisha utekelezaji wa mikakati ya maendeleo ya taasisi hiyo, kuongeza ubunifu katika utoaji wa huduma na kuendeleza ushirikiano na wadau mbalimbali ili kuhakikisha makumbusho yanaendelea kuwa kitovu cha elimu, uhifadhi wa urithi na maendeleo ya utalii nchini.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuendelea kuimarisha urithi wa taifa kama kichocheo cha maendeleo ya sekta ya utalii, sambamba na maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), yanayotarajiwa kuongeza fursa za kiuchumi kupitia utalii, utamaduni na huduma mbalimbali.