Kijiji cha Makumbusho

Kijiji cha Makumbusho ni makumbusho ya wazi iliyoanzishwa mwaka 1967 kwa lengo la kukusanya, kutafiti na kuhifadhi utamaduni wa jamii za watanzania na hasa mitindo ya ujenzi wa nyumba za asili. Makumbusho hii inaonyesha maisha halisi ya watanzania hadi kufikia miongo michache iliyopita kupitia nyumba na vifaa walivyotumia. Baadhi ya nyumba zilizojengwa hapa hazitumiwi tena wakati nyumba zingine hutumiwa na wanajamii wengi waishio sehemu za vijijini zikiwa zimeboreshwa au kuondolewa uasili wake. Kwa mantiki hiyo uhifadhi wa nyumba za mwanzo (asili) unaofanywa na Makumbusho hii una mchango mkubwa kwa jamii na Taifa kwa ujumla. Kijiji cha Makumbusho kipo kitalu namba D kiwanja namba 7 & 8 eneo la Kijitonyama, Barabara ya Ali Hassan Mwinyi Mtaa wa Makaburi katika Wilaya ya Kinondoni Mkoa wa Dar es Salaam.

Tanzania ina zaidi ya jamii (makabila) 120 ambazo zina tamaduni anuai kila moja lakini pamoja na tofauti hizi jamii hizi huwasiliana kwa lugha moja ya Kiswahili. Vivyo hivyo jamii zote za Tanzania hujenga na kuishi katika nyumba za aina kuu tatu ambazo ni:-

Muundo asili na muonekano pamoja na ujuzi wa ujenzi wa nyumba za asili unategemea mambo anuai ikiwemo sababu za kijiografia, upatikanaji wa malighafi za ujenzi, umahiri, utamaduni wa jamii husika, sababu za kiusalama na ulinzi dhidi ya wanyama wakali. Vivyo hivyo wingi na muundo wa wakazi, ongezeko la watu, hali ya uchumi na mgawanyiko wa jamii husika huchangia kuwepo kwa ukubwa, umbo, uimara, utendaji pamoja na muundo na kiwango cha mabadiliko kwa nyumba husika.

Kijiji cha Makumbusho kinawapa fursa wageni kutembelea na kuona maisha ya jamii za Tanzania katika sehemu moja na kwa muda mfupi. Jionee nyumba za asili, vifaa vya asili, mboga za asili pamoja na uoto wa asili utembeleapo Kijiji cha Makumbusho. Jipatie vifaa anuai vya kazi za mikono, ngoma za asili na chakula cha asili mara utembeleapo Kijiji cha Makumbusho.