MAKUMBUSHO YA TAIFA LA TANZANIA YAENDELEA KUTANGAZA URITHI WA TAIFA KUPITIA KONGAMANO LA KIMATAIFA LA KISWAHILI NCHINI UFARANSA
PARIS, UFARANSA, Julai 7, 2026 – Makumbusho ya Taifa la Tanzania imeendelea kutangaza na kuhamasisha urithi wa Taifa katika ngazi ya kimataifa kupitia ushiriki wake katika Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililofanyika kuanzia tarehe 4 hadi 7 Julai 2026 jijini Paris, nchini Ufaransa.
Ushiriki huo unaakisi dhamira ya Makumbusho ya Taifa la Tanzania ya kutekeleza wajibu wake wa kuhifadhi, kulinda, kufanya tafiti na kuendeleza urithi wa asili na utamaduni wa Tanzania, sambamba na kuitangaza nchi katika majukwaa ya kimataifa kupitia urithi wake wa kiutamaduni.
Katika kongamano hilo, Makumbusho ya Taifa la Tanzania limeonesha nafasi muhimu ya lugha ya Kiswahili kama sehemu ya utambulisho wa Taifa, urithi wa kitamaduni na nyenzo muhimu ya kuhifadhi, kuendeleza na kurithisha historia, mila, desturi na maarifa ya jamii kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Aidha, ushiriki wa taasisi hiyo umeendelea kusisitiza mchango wa Makumbusho ya Taifa katika kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili kama nyenzo ya kuhifadhi urithi wa utamaduni na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha urithi wa Kiswahili duniani.
Makumbusho ya Taifa la Tanzania katika kongamano hilo imewakilishwa na Mhifadhi Mwandamizi wa Kijiji cha Makumbusho, Bi. Wilhemina Deogratious Joseph, ambaye ameshiriki katika mijadala ya kitaaluma na shughuli mbalimbali zilizolenga kuimarisha nafasi ya lugha ya Kiswahili, urithi wa utamaduni na ushirikiano wa kimataifa katika maendeleo ya jamii.
Kupitia ushiriki wake katika kongamano hilo, Makumbusho ya Taifa la Tanzania linaendelea kutekeleza azma ya Serikali ya kuitangaza Tanzania kimataifa kwa kutumia urithi wa historia na utamaduni kama nyenzo ya kuimarisha diplomasia ya utamaduni, kukuza utalii wa urithi na kuhifadhi utambulisho wa Taifa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

