MAKUMBUSHO YA TAIFA KWA KUSHIRIKIANA NA KIDS TECH FESTIVAL YAWEZESHA WATOTO NA VIJANA KUPATA UZOEFU WA TEKNOLOJIA
Dar es Salaam, Agosti 16, 2026 — Makumbusho ya Taifa ya Tanzania, kwa kushirikiana na Kids Tech Festival Tanzania, imeandaa onesho la muda la teknolojia lililolenga kuwajengea watoto na wanafunzi uelewa, ubunifu na ujuzi wa matumizi ya teknolojia katika maisha ya kila siku.
Onesho hilo, lililofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 15 hadi 16 Agosti 2026 katika Ukumbi wa Muda wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni, Posta jijini Dar es Salaam, lilizinduliwa na Mgeni Rasmi, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA (ICT Commission), Dkt. Nkundwe Moses Mwasaga.
Zaidi ya wanafunzi 200 kutoka shule mbalimbali za Dar es Salaam walishiriki katika onesho hilo na kupata fursa ya kujifunza kwa vitendo kuhusu matumizi sahihi, salama na yenye tija ya teknolojia mbalimbali zinazotumika katika dunia ya sasa.
Miongoni mwa teknolojia zilizowasilishwa katika onesho hilo ni Akili Bandia (AI), Roboti, Usalama wa Taarifa Mtandaoni (Cyber Security), Internet of Things (IoT), Automation, Coding, Cloud Computing, SpaceTech, Virtual Reality (VR) na teknolojia ya 3D.
Kupitia mafunzo na maonesho hayo, wanafunzi pia walipata fursa ya kujifunza misingi ya utengenezaji wa programu za kompyuta, hali iliyowasaidia kukuza uwezo wa ubunifu, kufikiri kimantiki, kutatua changamoto na kutumia teknolojia kama nyenzo ya kubuni suluhisho kwa changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maisha ya kila siku.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Kaimu Mkuu wa Kituo cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni, Bi. Grace Manyasula, amesema matumizi ya maeneo na miundombinu ya Makumbusho kwa shughuli za kielimu na kiteknolojia ni sehemu muhimu ya kuendeleza dhana ya Makumbusho kuwa vituo vya kujifunzia, kubadilishana maarifa na kukuza ubunifu.
Bi. Manyasula amesema Makumbusho yana nafasi ya kipekee katika kuwawezesha wananchi, hususan watoto na vijana, kuelewa uhusiano kati ya urithi, historia, sayansi na maendeleo ya teknolojia, kwa kuwa Makumbusho huhifadhi na kuonesha ushahidi wa maendeleo ya teknolojia ya binadamu katika vipindi mbalimbali vya historia.
Ameongeza kuwa historia ya maendeleo ya binadamu nchini Tanzania inaonesha matumizi ya teknolojia mbalimbali tangu nyakati za kale, ikiwemo teknolojia za awali zilizogunduliwa katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, ambazo ni sehemu ya urithi unaohifadhiwa na Makumbusho ya Taifa.
Kwa upande wake, ushirikiano kati ya Makumbusho ya Taifa na Kids Tech Festival Tanzania umeonesha umuhimu wa kuunganisha sekta ya urithi na sekta ya teknolojia katika kuwapatia watoto na vijana mazingira rafiki ya kujifunza na kupata uzoefu wa vitendo.
Onesho hilo pia limekuwa fursa ya kuhamasisha matumizi ya teknolojia kwa njia salama na yenye tija, huku likiwajengea wanafunzi msingi wa kuelewa teknolojia zinazobadilisha dunia na kuwahamasisha kujiandaa kwa fursa za ajira, ujasiriamali na ubunifu katika uchumi wa kidijitali.
Makumbusho ya Taifa linaendelea kuhimiza ushirikiano na taasisi za elimu, teknolojia, ubunifu pamoja na wadau wengine katika kuendeleza programu zinazolenga kuwafikia watoto na vijana, na kutumia Makumbusho kama majukwaa ya elimu, ubunifu, maarifa na uzoefu wa vitendo.
Onesho la Kids Tech Festival katika Makumbusho ya Taifa limehitimisha kwa kuonesha umuhimu wa kuwajengea kizazi cha sasa uwezo wa kutumia teknolojia kwa ubunifu na uwajibikaji, sambamba na kuwafanya watoto na vijana kutambua kuwa teknolojia ni sehemu muhimu ya safari ya maendeleo ya binadamu na mustakabali wa jamii.

