MAKUMBUSHO YA TAIFA YASHIRIKIANA NA JAMII YA WAMASAI KUENZI MILA NA DESTURI
Kilimanjaro, Siha — 26 Agosti 2026
Makumbusho ya Taifa la Tanzania, kupitia Kanda ya Kaskazini, imeendelea kuimarisha ushirikiano na jamii katika juhudi za kuhifadhi, kuendeleza na kuenzi mila, desturi na urithi wa Kitanzania.
Katika kuendeleza juhudi hizo, Makumbusho ya Taifa ilishiriki katika sherehe za Rika za kusimika Kiongozi wa Jadi wa Kimasai, zilizofanyika tarehe 26 Agosti 2026 katika Kijiji cha Ormelili, Wilaya ya Siha, Mkoa wa Kilimanjaro.
Sherehe hizo zilikuwa sehemu muhimu ya kuenzi na kuendeleza mifumo ya kijamii, mila na desturi za jamii ya Wamasai, ambazo ni miongoni mwa urithi muhimu wa kitamaduni wa Tanzania.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Mkuu wa Kanda ya Kaskazini wa Makumbusho ya Taifa, Bi. Agness Robert, aliyeambatana na viongozi wa vituo, Bi. Elizabeth Solomon na Bw. Burah Akonay, pamoja na Afisa Masoko, Bi. Grace Naiman Mpogollo.
Ushiriki wa Makumbusho ya Taifa katika shughuli hiyo unaakisi dhamira ya Taasisi ya kushirikiana na jamii katika kutambua, kuhifadhi na kurithisha maarifa, mila, desturi na tamaduni za jamii mbalimbali nchini Tanzania kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Makumbusho ya Taifa inaendelea kutambua jamii kama wadau muhimu katika uhifadhi wa urithi wa taifa, hususan kupitia ushiriki wa moja kwa moja katika shughuli za kitamaduni na kijamii zinazolenga kuhakikisha urithi huo unaendelea kuwa sehemu ya utambulisho wa Taifa.
#TumerithishwaTuwarithishe
#NationalMuseumTanzania
#MaasaiCulture
#CulturalHeritage
#TanzaniaHeritage

