ZIARA YA RAIS WA TAASISI YA DIASPORA KUFUNGUA MILANGO YA UTALII MAKUMBUSHO YA TAIFA LA TANZANIA
DAR ES SALAAM, 26 Agosti 2026: Makumbusho ya Taifa la Tanzania imeendelea kufungua milango ya utalii wa kiutamaduni kwa wageni kutoka ndani na nje ya nchi, baada ya kupokea ujumbe kutoka Taasisi ya Maendeleo ya Diaspora wa Kiafrika (African Diaspora Development Institute – ADDI), unaoongozwa na Mwanzilishi na Rais wa Taasisi hiyo, Mheshimiwa Balozi Dkt. Arikana Chihombori-Quao kutoka Zimbabwe.
Ziara hiyo maalum iliyofanyika tarehe 26 Agosti 2026 katika Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Dar es Salaam, imelenga kuwapa wageni fursa ya kujifunza na kufahamu kwa kina historia, utamaduni na urithi wa Tanzania, pamoja na kutambua nafasi ya nchi katika historia na urithi mpana wa Afrika.
Kupitia ziara hiyo, wageni walipata fursa ya kutembelea na kujifunza kuhusu maonesho na historia mbalimbali zinazohifadhiwa na Makumbusho ya Taifa, hatua inayochangia kuongeza uelewa kuhusu utajiri wa urithi wa Tanzania na uhusiano wake na historia ya bara la Afrika.
Ushiriki wa wageni wenye asili ya Kiafrika kutoka nje ya bara katika kutembelea Makumbusho ya Taifa unaendelea kuwa sehemu muhimu ya juhudi za kukuza utalii wa urithi na utamaduni, huku ukifungua fursa za kujenga mahusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Waafrika wanaoishi nje ya bara.
Aidha, ziara hiyo inaakisi umuhimu wa diplomasia ya utamaduni katika kuitangaza Tanzania kimataifa, ambapo Makumbusho ya Taifa linatoa fursa kwa wageni kuelewa historia, tamaduni, mila na desturi za jamii mbalimbali za Tanzania kupitia makusanyo na maonesho yake.
Makumbusho ya Taifa linaendelea kutekeleza jukumu lake la kuhifadhi, kutunza, kutafiti na kuelimisha jamii kuhusu urithi wa taifa, huku likitumia urithi huo kama nyenzo ya kukuza utalii na kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na jamii mbalimbali duniani.
Ziara kama hiyo inatarajiwa kuchochea ongezeko la wageni wenye asili ya Kiafrika kutoka mataifa mbalimbali kutembelea Makumbusho ya Taifa na maeneo mengine ya urithi nchini Tanzania, kwa lengo la kujifunza kuhusu chimbuko, historia na utamaduni wa Afrika.
Kwa upande mwingine, ziara hiyo imeendelea kuimarisha nafasi ya Makumbusho ya Taifa kama kitovu cha historia, utamaduni na urithi wa Tanzania, pamoja na kuwa daraja linalowaunganisha Watanzania, Waafrika na Diaspora ya Afrika kupitia historia na urithi wao wa pamoja.
Makumbusho ya Taifa la Tanzania linaendelea kuwakaribisha wageni kutoka sehemu mbalimbali za dunia kujifunza, kugundua na kuenzi urithi wa Tanzania na Afrika kwa ujumla.

