Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Makumbusho ya Taifa la Tanzania

WANAFUNZI WAENDELEA KUNUFAIKA NA ELIMU YA URITHI WA KIUTAMADUNI KATIKA BANDA LA MAKUMBUSHO MAONESHO YA NANENANE

Imewekwa: 07 Aug, 2026
WANAFUNZI WAENDELEA KUNUFAIKA NA ELIMU YA URITHI WA KIUTAMADUNI KATIKA BANDA LA MAKUMBUSHO MAONESHO YA NANENANE

Dodoma, Agosti 6, 2026 – Makumbusho ya Taifa la Tanzania imeendelea kutoa elimu ya urithi kwa wanafunzi wanaotembelea banda lake katika Maonesho ya Wakulima (NaneNane) yanayoendelea mkoani Dodoma, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuhamasisha jamii, hususan vijana, kuthamini na kuhifadhi urithi wa Taifa.

Katika ziara zao, wanafunzi kutoka shule mbalimbali wamepata fursa ya kujifunza kuhusu historia ya Tanzania, urithi wa utamaduni, malikale na wajibu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania katika ukusanyaji, uhifadhi, utafiti na uendelezaji wa urithi wa Taifa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Mbali na kupata maelezo kutoka kwa wataalamu wa Makumbusho, wanafunzi wamejifunza kupitia programu shirikishi zinazojumuisha maonesho ya vielelezo vya kihistoria, shughuli za kujifunza kwa vitendo pamoja na mijadala inayochochea uelewa kuhusu umuhimu wa kuhifadhi urithi wa Taifa.

Akizungumza katika banda la Makumbusho, Mhifadhi wa Makumbusho amesema programu hizo zimeendelea kuvutia wanafunzi kutokana na mbinu za kujifunza kwa vitendo zinazowajengea uelewa mpana kuhusu historia, utamaduni na urithi wa Tanzania, sambamba na kuwahamasisha kuwa mabalozi wa uhifadhi wa urithi katika jamii zao.

Amesema ushiriki wa wanafunzi katika programu hizo unaunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha elimu ya urithi kwa vijana ili kuongeza uzalendo, kuthamini utambulisho wa Taifa na kuhamasisha ushiriki wa jamii katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za urithi wa Tanzania.

Makumbusho ya Taifa la Tanzania inaendelea kuwakaribisha wanafunzi, walimu, wazazi na wananchi wote kutembelea banda lake katika Maonesho ya NaneNane ili kujifunza kuhusu urithi wa Taifa, kupata elimu kutoka kwa wataalamu na kujionea vielelezo mbalimbali vinavyoonesha historia, utamaduni na urithi wa Tanzania.

#TumerithishwaTuwarithishe