Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Makumbusho ya Taifa la Tanzania

MAKUMBUSHO YA TAIFA LA TANZANIA YAJA NA MKAKATI MPYA 3P's KUELEKEA 2031 [3P's - PRESERVE, PROMOTE, PROSPER]

Imewekwa: 27 Oct, 2026
MAKUMBUSHO YA TAIFA LA TANZANIA YAJA NA MKAKATI MPYA 3P's KUELEKEA 2031  [3P's - PRESERVE, PROMOTE, PROSPER]

Makumbusho ya Taifa ya Tanzania (NMT) imeanza safari mpya ya mabadiliko ya kifikra na kimfumo, kufuatia kuandaliwa kwa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano unaolenga kuimarisha thamani na mchango wa makumbusho nchini.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo rejea kwa watumishi, yaliyofanyika katika kituo cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni tar 26-27 Oktoba 2026. Mwenyekiti wa Bodi ya NMT, Dkt. Oswald Masebo, alisema kuwa, imefurahishwa na mtazamo mpya wa NMT wa kuondokana na fikra za zamani zilizojikita kwenye uhifadhi pekee na badala yake NMT sasa imejipanga kuimarisha na kutekeleza majukumu mapana zaidi ya kutangaza, kukuza, na kuimarisha historia na urithi wa taifa.

"Ni lazima tutoke kwenye mtazamo wa kuwa wahifadhi tu wa vitu vya kale. Jukumu letu jipya na la msingi ni kutangaza na kukuza urithi wetu ili uwe na tija kwa jamii na ujenge hisia za uzalendo na kujivunia Taifa letu," alisema Dkt. Masebo.

Vilevile, Dkt. Masebo alieleza umuhimu wa Makumbusho ya Taifa kusimulia historia ya Tanzania kupitia mtazamo wa Kitanzania. Alifafanua kuwa kwa muda mrefu, sehemu kubwa ya historia ya Afrika na Tanzania imekuwa ikisimuliwa kupitia mtazamo wa nje, jambo linalopaswa kurekebishwa mara moja. 

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa NMT Dkt Noel Luoga alisema NMT imejipanga kutumia ubunifu na kushirikishaji wanataaluma katika kuandaa maonesho mapya. Akifafanua jinsi NMT ilivyojipanga kuondoa athari za ukoloni katika muundo na maonesho ya makumbusho, amesisitiza kuwa NMT itatumia watafiti, wanahistoria, na wataalamu wa ndani ili kuleta  mabadiliko yenye tija katika kuboresha maonesho yetu ili yawe na uhalisia wa Taifa letu. 
Amesisitiza kuwa ushirikiano huo utasaidia kuunda maonesho yenye mvuto wa kisayansi, kiutamaduni na kifalsafa hatua itakayochochea hisia za watazamaji, kukuza uzalendo na kuvutia wageni wengi zaidi kutembelea makumbusho.

Akihitimisha hotuba yake, Dkt. Masebo aliupongeza uongozi wa NMT kwa kuandaa Mpango Mkakati Mpya unaotoa dira thabiti ya mabadiliko. Amewataka watumishi wote kutumia fursa ya mafunzo hayo kujipanga upya kikazi na kimkakati, ili kuwa chachu ya mapinduzi haya makubwa katika kukuza utalii wa sekta ya utamaduni na urithi wa taifa.