Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Makumbusho ya Taifa la Tanzania

NMT YAIMARISHA UWEZO WA WATUMISHI KATIKA KINGA NA TAHADHARI DHIDI YA MAJANGA YA MOTO

Imewekwa: 03 Nov, 2026
NMT YAIMARISHA UWEZO WA WATUMISHI KATIKA KINGA NA TAHADHARI DHIDI YA MAJANGA YA MOTO

Dar es Salaam, 02 Novemba 2026. 

Makumbusho ya Taifa la Tanzania (NMT) imeendesha mafunzo ya kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto kwa watumishi wake, ikiwa ni sehemu ya juhudi za taasisi hiyo kuimarisha usalama wa watumishi, wageni, mali na miundombinu ya taasisi.

Mafunzo hayo yamefanyika Jumatatu, tarehe 02 Novemba 2026, katika ukumbi wa mikutano wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni, Posta, jijini Dar es Salaam, na kufunguliwa rasmi na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Dkt. Noel Lwoga.

Katika ufunguzi huo, Mkurugenzi Mkuu aliambatana na Mkurugenzi wa Huduma na Shirika, Bw. Zakkarriya Kyera, pamoja na Mkuu wa Utawala na Rasilimaliwatu, Bi. Renalda Lyimo.

Mafunzo hayo yaliendeshwa na wataalamu kutoka Jeshi la Zima Moto na Uokoaji, wakiongozwa na A/INSP Mohamed Selungwi, FC Eliamani Mwanga na FC Jofrey Sindika, ambao waliwapatia watumishi elimu na uelewa kuhusu visababishi vya majanga ya moto, aina mbalimbali za moto, matumizi sahihi ya vifaa vya kuzimia moto pamoja na taratibu za kufuata wakati wa kukabiliana na matukio ya dharura.

Aidha, mafunzo hayo yalilenga kuwajengea watumishi uwezo wa kutambua viashiria vya hatari ya moto, kuchukua tahadhari za mapema na kutumia vifaa vya kuzimia moto kwa usahihi ili kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na majanga hayo.

Kupitia mafunzo hayo, Makumbusho ya Taifa la Tanzania inaendelea kuimarisha mifumo ya usalama kazini kwa kujenga uelewa na utayari wa watumishi katika kuzuia na kukabiliana na majanga ya moto, sambamba na kuhakikisha mazingira salama kwa shughuli za uhifadhi wa urithi wa taifa na utoaji wa huduma kwa wananchi na wageni.