Makumbusho na Familia ya Mwalimu Nyerere Kuimarisha Ushirikiano wa Utalii Kupitia One Stop Centre.
Dar es Salaam, 20 Novemba 2026
Makumbusho ya Taifa la Tanzania (NMT), kwa kushirikiana na Familia ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, imefanya kikao cha majadiliano kuhusu mpango wa kuanzisha Kituo cha Pamoja cha Huduma kwa Watalii na Wageni (One Stop Centre), kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma na uzoefu wa wageni wanaotembelea maeneo ya urithi wa kihistoria nchini.
Kikao hicho kimefanyika tarehe 20 Novemba 2026 katika Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni, Dar es Salaam, kikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa NMT, Dkt. Noel Lwoga, pamoja na mwakilishi wa Familia ya Mwalimu Nyerere, Bw. Madaraka Nyerere.
Majadiliano hayo yalilenga kuendeleza msingi wa ushirikiano kati ya pande hizo mbili katika kuanzisha kituo hicho, kitakachokuwa na jukumu la kurahisisha upatikanaji wa huduma na taarifa kwa watalii na wageni, pamoja na kuboresha uratibu wa huduma zinazotolewa katika maeneo husika.
Uanzishwaji wa kituo hicho ni miongoni mwa hatua zinazolenga kuimarisha ushirikiano kati ya NMT na Familia ya Mwalimu Nyerere katika kuhifadhi, kutangaza na kukuza urithi wa kihistoria wa Taifa.
Aidha, mpango huo unatarajiwa kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, kuboresha uzoefu wa wageni na kuimarisha thamani ya maeneo ya kihistoria kama vivutio muhimu vya utalii nchini.
Kupitia ushirikiano huo, NMT inaendelea kutekeleza dhamira yake ya kulinda, kuendeleza na kutangaza urithi wa asili, historia na utamaduni wa Tanzania kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

