Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Makumbusho ya Taifa la Tanzania

WAZIRI WA ZANZIBAR ATEMBELEA KIJIJI CHA MAKUMBUSHO KUPATA UZOEFU WA UANZISHWAJI WA KIJIJI CHA UTAMADUNI ZANZIBAR

Imewekwa: 18 Nov, 2026
WAZIRI WA ZANZIBAR ATEMBELEA KIJIJI CHA MAKUMBUSHO KUPATA UZOEFU WA UANZISHWAJI WA KIJIJI CHA UTAMADUNI ZANZIBAR

Dar es Salaam, 17 Novemba 2026

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Dkt. Riziki Pembe, ametembelea Kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujifunza uzoefu wa uanzishaji, uendeshaji na usimamizi wa makumbusho ya kijiji, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuanzisha kivutio cha aina hiyo visiwani Zanzibar.

Kijiji cha Makumbusho kinachosimamiwa na Makumbusho ya Taifa la Tanzania (NMT), ni miongoni mwa vivutio muhimu vya urithi wa utamaduni nchini vinavyotoa fursa kwa wageni kujifunza historia, mila, desturi, usanifu wa makazi ya jadi na maisha ya jamii mbalimbali za Kitanzania.

Katika ziara hiyo, Mhe. Dkt. Pembe aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Ndugu Matar Zahor Masoud, na kupokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Dkt. Noel Biseko Lwoga, pamoja na watumishi wa taasisi hiyo.

Akielezea madhumuni ya ziara hiyo, Mhe. Dkt. Pembe amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inalenga kujifunza kutoka kwa Makumbusho ya Taifa la Tanzania kuhusu mifumo na mbinu bora za kuanzisha na kuendesha Kijiji cha Utamaduni kitakachokuwa na jukumu la kuhifadhi, kuendeleza na kutangaza urithi wa kipekee wa kihistoria na kiutamaduni wa Zanzibar.

Amesema kuwa kupitia ziara hiyo amepata fursa ya kujionea namna Kijiji cha Makumbusho kinavyotekeleza majukumu yake ya kuhifadhi urithi wa taifa kupitia makazi ya jadi, vifaa vya asili, mila na desturi za jamii mbalimbali, pamoja na shughuli zinazowezesha wananchi na wageni kujifunza na kuthamini utajiri wa utamaduni wa Tanzania.

Uzoefu huo unatarajiwa kuwa chachu katika maandalizi ya kuanzishwa kwa Kijiji cha Utamaduni Zanzibar, ambacho kitakuwa jukwaa muhimu la kuhifadhi na kutangaza urithi wa visiwa hivyo, kukuza utalii wa utamaduni na kutoa fursa za kiuchumi kwa jamii.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Dkt. Noel Biseko Lwoga, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizo katika kubadilishana uzoefu, maarifa na utaalamu wa uhifadhi, usimamizi na uendelezaji wa urithi wa kihistoria na kiutamaduni.

Ameeleza kuwa Makumbusho ya Taifa la Tanzania iko tayari kuendeleza ushirikiano wa kitaalamu katika maeneo mbalimbali yanayohusu uhifadhi na uendelezaji wa urithi, kwa kuzingatia umuhimu wa makumbusho katika kutoa elimu, kukuza utalii wa utamaduni na kurithisha maarifa kwa vizazi vijavyo.

Ziara hiyo ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kitaasisi kati ya Makumbusho ya Taifa la Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, hususan katika kukuza uhifadhi na matumizi endelevu ya urithi wa taifa kama nyenzo ya elimu, utalii wa utamaduni na maendeleo ya jamii.