Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Makumbusho ya Taifa la Tanzania

MAKUMBUSHO YA TAIFA LA TANZANIA YAZINDUA KAMATI YA UONGOZI NA UHIFADHI KUIMARISHA UHIFADHI WA URITHI WA TAIFA

Imewekwa: 03 Jul, 2026
MAKUMBUSHO YA TAIFA LA TANZANIA YAZINDUA KAMATI YA UONGOZI NA UHIFADHI KUIMARISHA UHIFADHI WA URITHI WA TAIFA

Dar es Salaam - Julai 2, 2026

Makumbusho ya Taifa la Tanzania (NMT) imezindua rasmi Kamati ya Uongozi na Uhifadhi (Management and Conservation Steering Committee), hatua muhimu inayolenga kuimarisha uhifadhi, ulinzi na usimamizi endelevu wa urithi wa utamaduni na historia wa Tanzania.

Kamati hiyo yenye wajumbe 11 imeundwa kutoa uongozi wa kimkakati, ushauri wa kitaalamu na usimamizi wa shughuli za uhifadhi zinazotekelezwa na taasisi, sambamba na kutekeleza dhamira ya Makumbusho ya Taifa ya kuhifadhi, kulinda na kuendeleza urithi wa taifa.

Kamati itafanya kazi chini ya usimamizi wa Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Dkt. Noel Biseko Lwoga, huku Sekretarieti yake ikiratibiwa na Mkurugenzi wa Makumbusho na Mambo ya Kale kwa kushirikiana na Kitengo cha Programu, Elimu na Maendeleo pamoja na Kitengo cha Utafiti, Uhifadhi na Ulinzi.

Aidha, Kamati inajumuisha Wakuu wa Kanda za Kusini na Mashariki, Wakuu wa Vitengo vya Sheria, Masoko na Uhusiano kwa Umma, Mipango, pamoja na wataalamu waandamizi wa Utafiti na Uhifadhi.

Katika kipindi chake cha miaka mitatu, Kamati hiyo itaongoza maandalizi ya miongozo ya kitaifa ya uhifadhi, mikakati ya muda mrefu, sera na nyaraka mbalimbali za kitaasisi zitakazoweka viwango vya kitaalamu katika usimamizi na uhifadhi wa urithi wa taifa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Dkt. Noel Biseko Lwoga, alisema kuanzishwa kwa Kamati hiyo ni hatua ya kihistoria kwa taasisi na sekta ya uhifadhi nchini.

"Kuundwa kwa Kamati hii kunaashiria mwanzo wa hatua mpya ya kuimarisha viwango vya uhifadhi na uwezo wa taasisi katika kulinda urithi wa taifa. Ni uthibitisho wa dhamira yetu ya kuhakikisha urithi wa Tanzania unahifadhiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo," alisema Dkt. Lwoga.

Kwa upande wake, Katibu wa Kamati hiyo, Bi. Adelaide Salema, alisema kuanzishwa kwa Kamati hiyo kunaweka msingi imara wa kuimarisha ubora wa shughuli za uhifadhi nchini.

"Kamati hii inaweka mfumo madhubuti wa uongozi na uratibu utakaowezesha kuimarisha viwango vya uhifadhi, kuongeza ushirikiano wa kitaalamu na kuhakikisha urithi wetu unalindwa kwa kuzingatia misingi bora ya uhifadhi," alisema.

Kuundwa kwa Kamati hiyo kunakuja wakati ambapo Makumbusho ya Taifa la Tanzania linaendelea kutekeleza majukumu yaliyopanuliwa chini ya Sheria mpya ya Mambo ya Kale, ambayo imeipa taasisi jukumu la kusimamia, kulinda na kuhifadhi zaidi ya maeneo 107 ya makumbusho, historia na urithi wa taifa yaliyopo nchini.

Kupitia Kamati hii ya Uongozi na Uhifadhi, Makumbusho ya Taifa la Tanzania kinaimarisha uwezo wake wa kutekeleza majukumu hayo kwa kuzingatia viwango vya kimataifa na mbinu bora za uhifadhi, kwa lengo la kuhakikisha urithi wa Tanzania unaendelea kulindwa na kuhifadhiwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.