BANDA LA MAKUMBUSHO YA TAIFA LA TANZANIA LAENDELEA KUVUTIA MAELFU YA WAGENI KATIKA MAONESHO YA 50 YA KIMATAIFA YA BIASHARA (SABASABA 2026)
Dar es Salaam, Julai 3, 2026
Banda la Makumbusho ya Taifa la Tanzania (NMT) limeendelea kuwa miongoni mwa vivutio vikubwa katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (Sabasaba 2026), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, likivutia maelfu ya wananchi, wadau na wageni kutoka maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi.
Wageni wanaotembelea banda hilo wanapata fursa ya kujifunza kuhusu historia, utamaduni na urithi wa Tanzania kupitia maonesho ya vielelezo vya kihistoria, malikale na taarifa mbalimbali zinazoonesha utajiri wa urithi wa taifa. Maonesho hayo yanalenga kuongeza uelewa wa umma kuhusu umuhimu wa kuhifadhi na kuendeleza urithi wa Tanzania kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Katika kipindi chote cha maonesho, wataalamu wa Makumbusho ya Taifa wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi, ikiwemo usimamizi wa makumbusho, uhifadhi wa urithi wa utamaduni na historia, pamoja na nafasi ya urithi katika kukuza utalii endelevu na maendeleo ya taifa.
Aidha, wageni wanapata taarifa kuhusu makumbusho na maeneo mbalimbali ya urithi yanayosimamiwa na Makumbusho ya Taifa la Tanzania yaliyopo katika kanda na mikoa mbalimbali nchini. Kupitia maonesho hayo, taasisi inaendelea kuhamasisha wananchi kutembelea vivutio vya urithi wa taifa na kushiriki katika juhudi za kuendeleza utalii wa ndani, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Tanzania kuelekea Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).
Mbali na kutoa elimu, banda la Makumbusho ya Taifa limeendelea kuwa jukwaa la kuhamasisha wananchi kutambua mchango wa urithi wa historia na utamaduni katika kujenga utambulisho wa taifa, kukuza uchumi kupitia utalii na kuhifadhi historia kwa vizazi vijavyo.
Makumbusho ya Taifa la Tanzania inaendelea kuwakaribisha wananchi wote kutembelea banda lake katika Maonesho ya Sabasaba 2026 ili kujionea hazina ya urithi wa taifa, kupata elimu kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi na kujifunza nafasi ya urithi wa Tanzania katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

