Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Makumbusho ya Taifa la Tanzania

MAKUMBUSHO YA TAIFA LA TANZANIA  KUIMARISHA TAFITI ZA MALIKALE ILI KUONGEZA MIKUSANYO NA UELEWA KUHUSU HISTORIA NA URITHI WA TAIFA

Imewekwa: 16 May, 2026
MAKUMBUSHO YA TAIFA LA TANZANIA  KUIMARISHA TAFITI ZA MALIKALE ILI KUONGEZA MIKUSANYO NA UELEWA KUHUSU HISTORIA NA URITHI WA TAIFA

Katika Mawasilisho ya  Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia waziri wake Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akiwa Bungeni jijini Dodoma  Mei 15, 2026. Amesema “Shirika limeendelea kuimarisha tafiti za malikale na makumbusho ili kuongeza mikusanyo na uelewa kuhusu historia, mila, desturi na urithi wa Taifa. Jumla ya tafiti 18 zimefanyika katika maeneo ya malikale na makumbusho kwa kushirikisha wadau wa uhifadhi na uendelezaji malikale nchini. Kupitia tafiti hizo, machapisho matatu (3) ya kisayansi yameandaliwa na vibali 11 vya utafiti vimetolewa kwa wananchi waliopo maeneo ya Kahama, Mpwapwa, Moshi, Korogwe, Tanga, Morogoro na Bagamoyo. Aidha, Shirika limeratibu warsha mbili (2) za kitafiti kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Chuo Kikuu cha Hannover cha Ujerumani na kusimamia kazi miradi 521 iliyofanywa na wanafunzi wa shule za sekondari 150 zilizopo mikoa ya Dar es Salaam (43), Lindi (20) Arusha (25), Ruvuma (32) na Mara (30).”

Katika kuimarisha kumbukumbu za Taifa na kuhifadhi ushahidi wa kihistoria, Makumbusho ya Taifa la Tanzania imeongeza wigo wa uhifadhi wa historia na malikale kwa kukusanya mikusanyo mipya 678 inayohusiana na historia, mila, akiolojia, palaentolojia na biolojia hivyo kufanya idadi ya mikusanyo iliyopo Makumbusho ya Taifa kufikia 628,135. Kati ya mikusanyo hiyo iliyokusanywa, 287 ni noti za kale, 10 ni mikusanyo ya baiolojia, 152 ni mikusanyo ya Paleontolojia, 14 ni mikusanyo kutoka Meli ya Kihistoria ya MV Liemba, 214 ni mikusanyo ya mila. Pia, Shirika lilipokea mkusanyo wa gari moja (1) aina ya Mercedes-Benz iliyotumiwa na Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, Rais wa Awamu ya Tatu, katika kipindi cha pili cha utawala wake (2000-2005).

Aidha, Shirika limefanya uchambuzi wa mikusanyo 143,693 yenye asili ya Akiolojia na Palaentolojia na kuiorodhesha katika kanzidata. Mikusanyo hiyo imetokana na tafiti zilizofanyika katika maeneo ya Ziwa Eyasi, Ngorongoro, Seronera, Ndutu, Mumba, Kilwa Kisiwani, Mafia Kisimani, Tongoni na Pangani. Aidha, kati ya mikusanyo hiyo iliyochambuliwa, mikusanyo 306 imesajiliwa katika mfumo wa kidijitali wa usimamizi na uhifadhi wa kumbukumbu unaojulikana kama Digital Records and Archives Management Preservation System -DRAMPS unaorahisisha uhifadhi na upatikanaji wa haraka wa taarifa za Malikale.

Katika kuhakikisha jamii inashiriki kikamilifu katika uhifadhi wa urithi wa Taifa, Shirika limeratibu na kuendesha mikutano 32 ya wadau wa uhifadhi malikale. Mikutano hiyo ilifanyika katika Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni (5), Nandete (3), Mtwara Mikindani (2), Majimaji Songea (6), Lindi Mjini (3), Tendaguru (2), Arusha (6), Kua Mafia (1), Mbuamaji (1), Pangani (1), Kilimanjaro (1) na Ujiji-Kigoma (1). Aidha, Shirika limewezesha jamii za kitanzania kukutana katika Kijiji cha Makumbusho - Dar es Salaam ili kuenzi na kutunza mila na desturi zao. Jamii tano (5) zikiwemo za Wamasai, Wasambaa, Wabembe, Wafipa na Wanyakyusa zimekutana na kujadili namna ya kuendelea kutunza desturi zao ikiwa ni sehemu ya utalii wa utamaduni. Moja ya mikakati ya jamii hizo ni kuhifadhi na kuenzi utamaduni wa usanifu wa jadi katika ujenzi wa nyumba za asili kwa kaya zao, kufanya matamasha ya jamii zao na kuwasilisha mikusanyo katika Kijiji cha Makumbusho.

Shirika limeendelea kuhamasisha umma wa watanzania kuhifadhi historia zao na kuzirithisha kutoka kizazi kimoja kwenda kingine. Katika kutekeleza jukumu hilo, Shirika limetoa ushauri kwa Taasisi sita (6) na jamii sita (6) kuanzisha Makumbusho binafsi. Taasisi zilizohamasishwa zinajumuisha; Wizara ya Nishati kuhusu uanzishwaji wa Makumbusho ya historia ya mradi wa Bwawa la kufua Umeme la Mwalimu Julius Nyerere, Mahakama Kuu ya Tanzania kuhusu kuanzisha Makumbusho ya Mahakama, Mkoani Dodoma; Chuo cha Ulinzi cha Taifa kuhusu historia ya Ulinzi nchini, Wilaya ya Maswa kuhusu kuanzisha Makumbusho ya tiba asili katika kijiji cha Bukigi,Wilaya ya Ukerewe kuhusu kuanzisha Makumbusho ya Historia na Utamaduni na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino kuhusu kuanzisha makumbusho ya historia ya chuo hicho.

Katika kuelimisha jamii na kuhamasisha watalii wa ndani na nje ya nchi kutembelea Makumbusho, Shirika limekamilisha Onesho Jipya la kudumu la ndege ya kwanza ya Serikali aina ya Jet, Fokker-28-5H- CCM iliyotumiwa na Marais wa nchi kwa Awamu Tano kuanzia mwaka 1978 hadi 2018. Vile vile, Shirika limeandaa na kuendesha maonesho ya muda ya kimakumbusho 10 yaliyotembelewa na wageni 102,420 yakiwemo Onesho la Fahari ya Tanzania katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba); Onesho la Picha za Msanii Doreen Mandawa msanii Maarufu raia wa Scotland alieishi Tanzania kwa miongo 5 akifundisha na kukuza kizazi cha wasanii wa uchoraji; Onesho la mapishi ya asili ya kitanzania Cke Patch Picnic Tourism in Museum; Onesho la Chakula cha asili cha Japani I Love Sushi kwa ushirikiano na Serikali ya Japan; Onesho la historia ya ujezi wa reli ya TAZARA kwa kushirikiana na Makumbusho ya Taifa la China kupitia Ubalozi wa China nchini; Onesho la Mchango wa Urusi katika Harakati za Ukombozi wa Afrika kwa kushirikiana na Kituo cha Utamaduni cha Ubalozi wa Urusi nchini; na Onesho la Ubunifu 9th Edition of the Day of the Italian Photo Design in the World. Shirika limeshiriki maonesho ya kitalii ya ITB Berline. Aidha, maudhui ya kidijitali matano (5) yameandaliwa na kuwekwa kwenye vifaa vya kidijitali vilivyopo kwenye Onesho la Kudumu la Mwl. Nyerere, Butiama.

Makumbusho ya Taifa la Tanzania imeanza maboresho ya mifumo ya kutoa huduma ya kidijitali ambapo linajenga Mfumo Jumuishi wa Huduma za Makumbusho Self Service Portal utakaorahisisha upatikanaji wa huduma kwa wageni. Mfumo huu utatoa huduma nane (8) kwa wageni ambazo ni vibali vya utafiti, viingilio, kupiga picha mnato na mjongeo, huduma ya kufanya utafiti ndani ya makumbusho, huduma ya kuongoza watalii, ukodishaji wa kumbi na maombi ya kuanzisha makumbusho ambapo moduli za Vibali vya utafiti na Viingilio zimekamilika.

Shirika limeendesha matamasha matatu (3) na matukio sita (6) ya kuhamasisha uhifadhi na utalii wa malikale likiwemo Tamasha la Kumbukizi ya Vita vya Majimaji Songea, Tamasha la Jamii ya Wazaramo katika Kijiji cha Makumbusho na Tamasha la Entabuko Mkoani Kagera. Aidha, programu 15 za kimakumbusho zimefanyika ikiwemo programu ya Museum Art Explosion, programu kwa wanafunzi wa vyuo vikuu (University Museum Hub) na programu ya simulizi za kimakumbusho (Museum Talk) inayorushwa kupitia mitandao ya kijamii.

Baada ya kuwasilisha hotuba yake Mhe. Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Kijaji alipata fursa ya kutembelea Makumbusho inayotembea kujionea mikusanyo mbalimbali ya historia, utamaduni na urithi wa Taifa yanayotolewa na Makumbusho ya Taifa la Tanzania kwa lengo la kuhamasisha utalii wa ndani na kuhifadhi historia ya Tanzania.