NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII AIPONGEZA MAKUMBUSHO YA TAIFA KWA KUHIFADHI NA KUTANGAZA URITHI WA TAIFA
DAR ES SALAAM, Julai 6, 2026 – Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Hamad Hassan Chande, ameipongeza Makumbusho ya Taifa la Tanzania kwa juhudi zake za kuhifadhi, kulinda na kutangaza urithi wa historia, tamaduni na malikale za Taifa, akieleza kuwa kazi hiyo ina mchango mkubwa katika kuimarisha utambulisho wa Taifa na kukuza utalii.
Mheshimiwa Chande ametoa pongezi hizo alipotembelea Banda la Makumbusho ya Taifa la Tanzania katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), maarufu kama SABASABA, yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Amesema Makumbusho ya Taifa limeendelea kutekeleza kwa ufanisi jukumu lake la kuhifadhi na kuendeleza urithi wa Taifa sambamba na kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa historia, tamaduni na malikale katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na sekta ya utalii.
Aidha, ameitaka taasisi hiyo kuendelea kutumia ubunifu na teknolojia za kisasa katika kutangaza vivutio vya urithi wa utamaduni na historia ili kuongeza idadi ya wananchi na watalii wanaotembelea makumbusho mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Chande amesema hatua hiyo itaiwezesha Tanzania kunufaika zaidi na fursa zinazotokana na ukuaji wa sekta ya utalii, hususan kuelekea Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), ambapo nchi inatarajiwa kupokea wageni wengi kutoka mataifa mbalimbali.
Kwa upande wake, Makumbusho ya Taifa la Tanzania inaendelea kutumia Maonesho ya SABASABA kama jukwaa la kuelimisha umma kuhusu historia ya Tanzania, urithi wa utamaduni wa Kiswahili, masalia ya dainosaria, malikale na vivutio vingine vya kipekee vinavyoitambulisha Tanzania katika ramani ya utalii wa urithi duniani.
Makumbusho ya Taifa la Tanzania linawakaribisha wananchi na wadau mbalimbali kutembelea banda lake katika Maonesho ya SABASABA ili kujionea urithi wa Taifa, kupata elimu kuhusu historia ya Tanzania na kufahamu huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo.

