Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Makumbusho ya Taifa la Tanzania

Mwenyekiti wa Bodi ya Ukaguzi ya Jamhuri ya Indonesia (BPK), Dkt. Isma Yatun, Atembelea Makumbusho ya Taifa la Tanzania

Imewekwa: 19 Jun, 2026
Mwenyekiti wa Bodi ya Ukaguzi ya Jamhuri ya Indonesia (BPK), Dkt. Isma Yatun, Atembelea Makumbusho ya Taifa la Tanzania

Dar es Salaam, 17 Juni 2026 – Mwenyekiti wa Bodi ya Ukaguzi ya Jamhuri ya Indonesia (BPK), Dkt. Isma Yatun, akiwa ameambatana na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Bw. Charles E. Kichere, ametembelea Makumbusho ya Taifa la Tanzania katika vituo vya Posta na Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo, Dkt. Yatun alipata fursa ya kujionea historia ya Tanzania, urithi wake wa kitamaduni pamoja na vivutio mbalimbali vya utalii wa urithi vinavyohifadhiwa na Makumbusho ya Taifa la Tanzania. Aidha, alieleza kufurahishwa na utajiri wa urithi wa Tanzania na namna unavyochangia kuitangaza nchi kama moja ya maeneo muhimu ya utalii wa urithi duniani.

Ziara hiyo iliratibiwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT), ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano kati ya Taasisi Kuu za Ukaguzi za Tanzania na Indonesia. Vilevile, ziara hiyo ilitoa fursa ya kuitangaza Tanzania kupitia vivutio vyake vya kipekee vya urithi kwa wageni wa kimataifa.

Makumbusho ya Taifa la Tanzania linaendelea kuwa miongoni mwa taasisi muhimu zinazohifadhi na kuendeleza urithi wa taifa kwa kuhifadhi historia, tamaduni, sanaa na maendeleo ya Tanzania kuanzia nyakati za kale hadi sasa. Kupitia mikusanyo yake ya kihistoria, kiakiolojia, kibaolojia na kiutamaduni, makumbusho huwapatia wageni fursa ya kujifunza historia ya Tanzania na kutambua mchango wake katika maendeleo ya ustaarabu na historia ya dunia.

Ziara ya Dkt. Isma Yatun ni kielelezo cha nafasi muhimu ya urithi wa Tanzania katika kuimarisha mahusiano ya kimataifa, diplomasia ya utamaduni, na kukuza utalii wa urithi unaochangia maendeleo ya uchumi wa taifa.

"Jifunze Historia Yetu, Furahia Urithi Wetu, Tembelea Makumbusho ya Taifa la Tanzania."