Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Makumbusho ya Taifa la Tanzania

Asili ya jina la mji wa Songea inatokana na jina la msaidizi wa chifu mkuu?

Imewekwa: 02 Jan, 2024
Asili ya jina la mji wa Songea inatokana na jina la msaidizi wa chifu mkuu?

Kabla ya vita vya Majimaji na kufahamika kwa mashujaa mbalimbali katika mji huu wa Songea eneo hili lilikuwa linafahamika kama mji wa Ndonde, jina hili la ndonde limetokana na kabila la watu walioishi mwanzoni kabla ya ujio wa wangoni katika eneo hili waliofahamika kama Wandonde.

Wandonde wa zamani ndio walioishi kwa muda mrefu katika eneo hili la mji wa Ndonde mpaka walipoingia Wangoni miaka ya 1840 ambapo baada ya kuingia Wangoni walifanya uvamizi katika eneo hili la mji wa ndonde na kupigana na wenyewi waliowakuta katika eneo hili, kutokana na ujuzi wa vita pamoja na nguvu walizokuwa nazo wangoni ilipelekea Wandonde kushindwa vita hiyo ya ndani ndipo hapo Wandonde walilazimika kuhama katikati ya mji wa Ndonde na kuelekea maeneo mengine,

Wandonde hao wa mwanzoni waligawanyika katika makundi mawili ambapo walipatikana Wandendeule wa sasaivi waliokwenda kuishi maeneo ya Namtumbo na jina hili la Wandendeule linatokana na msemo unaofahamika kama ndendeule msemo huu ukiwa unamaanisha tufanyeje,  maana baada ya kushindwa vita dhidi ya Wangoni hawakuwa na namna ya kufanya na kupelekea kuhama katika mji wao wa ndonde na kuhamia eneo lingine kutokana na mgawanyiko huu wa wandonde ambao ni wandendeule wa sasa lilizaliwa kabila jingine pia ambalo nalo lilijitenga kutoka wandonde waliokwenda kuishi namtumbo nao wakaelekea maeneo ya milimani wakafahamika kwa jina la Wamatengo ambapo wamatengo ilimaanisha watu wa milimani kwa sasa ni maeneo ya mbinga moja ya wilaya inayopatikana mkoa wa Ruvuma.

Nduna Songea Luwafu Mbano ni moja ya chifu msaidizi kati ya machifu 11 wasaidizi waliokuwa wanamsaidia chifu mkuu aliyefahamika kwa jina la Inkosi Mputa bin Gwazerapasi Gama, Nduna Songea Mbano ndiye aliyekuwa Msaidizi mkuu kati ya wasaidizi 11 wa Inkosi Mputa Gama na ndiye aliyepewa jukumu la kuwaongoza manduna wengine,  Taarifa zote zilikuwa zinamfikia yeye kwanza kabla ya kufika kwa chifu mkuu, Vilevile maelekezo yote yaliyokuwa yanatoka kwa chifu mkuu ilikuwa lazima afikishiwe nduna Songea kwanza na yeye kuwaagiza wasaidizi wengine, vilevile Nduna Songea Mbano ndiye aliyekuwa Jemedari mkuu akiwaongoza wenzake kipindi chote cha vita vya Majimaji katika eneo la Songea.

Nduna Songea Mbano amekuwa maarufu zaidi kuliko chifu mkuu (Inkosi) Mputa Gama bin Gwazerapasi kwa sababu mbalimbali: kwanza kabisa umaarufu mkubwa wa Nduna Songea umeonekana kipindi cha vita vya Majimaji  kutokana na mchango mkubwa alioutoa kipindi chote cha vita akiwa kama Nduna mkuu na jemedari mkuu wa vita hivyo, Pia alipata umaarufu kutokana na mambo aliyoyafanya ukilinganisha na yale aliyoyafanya chifu mkuu (Inkosi) Mputa Gama, Chifu Songea ndiye aliyetoa mbinu mbalimbali za upiganaji na kupanga wapiganaji wa vita hivyo katika eneo la Songea, ndiye mtu aliyehofiwa zaidi na Wajerumani kuliko mtu yeyote katika kipindi chote cha vita.

Chifu Songea alikuwa na ngome yake katika mapango ya mlima Chandamali ambayo Wajerumani hawakuweza kuiingia, alikuwa na maajabu mengi ikiwa kuweza kupotea kimiujiza mbele za watu, ndiye jemedari pekee wa vita ambaye Wajerumani walisumbuka sana kumkamata na ndiye mtu pekee aliyepigwa kitanzi mara tatu kwaajili ya kunyongwa na wajerumani bila mafanikio hivyo kutokana na mambo hayo mbalimbali aliyoyafanya na yaliyotokea yamepelekea yeye kuwa maarufu zaidi ya chifu mkuu Mputa Gama.