Historia

MIKUSANYO YA KIHISTORIA

Maonyesho ya historia ni miongoni mwa maonyesho yanayopatikana Makumbusho ya Taifa. Maonyesho ya historia yamegawanyika katika sehemu mbalimbali ikiwemo Historia ya Tanzania kabla ya kuja kwa wageni na baada ya ujio wa wageni, kipindi cha kupigania uhuru ( harakati za ukombozi ) kipindi cha Azimio la Arusha, mabadiliko ya kisiasa miaka ya 1990's, pamoja na mabadiliko yanayoendelea kuchukua sura mpya hivi sasa.

Kumbi hizi za historia katika mpangilio wake unamuwezesha mgeni na hata mwenyeji kuweza kujifunza na kuelewa vizuri historia ya Tanzania na Afrika kwa ujumla kabla ya kuja kwa wageni, uhusiano wao na vitu mbalimbali walivyokuwa wakibadilishana katika biashara, pia unyanyasaji wa Africa kama vile biashara ya utumwa ikiwa na lengo la kumfanya muafrika kama bidhaa na hii ilikuwa ni unyanyasaji wa hali ya juu..

Lakini pia wageni na wenyeji watapata kuelewa na kujifunza na kutambua jitihada mbalimbali zilizochukuliwa na waafrika kuweza kukabiliana na unyanyasaji / unyonyaji huo. kufikia miaka ya 1960's unaweza kuona nchi nyingi za Afrika zikiweza kupigania uhuru wao kutoka kwa wakoloni, ikiwemo Tanzania lakini baada ya uhuru Tanzania ikachukua sura mpya na kuanza kufanya mabadiliko katika sekta zote za kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Pia kuna maonyesho mbalimbali ya magari ya kihistoria, kama vile Austin Morris, Van Guards na Mercedes Benz E.300 yaliyotumiwa na baba wa Taifa mwl. J.K. Nyerere kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kuendeleza chama cha TANU, pia kuna Rolls Royce iliyotumika mwaka 1962 - 1970 Ambayo yako Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni. Pia maonyesho mengine kama kumbukumbu ya wahanga wa mashambulizi ya mabomu yaliyofanyika katika ubalozi wa marekani Tanzania, tarehe 07.08.1998. Wageni wapatao 12 walifariki katika tukio hilo na majeruhi 77 wakiwemo wafanyakazi wa ubalozi huo.

Makumbusho ya Taifa ndio sehemu pekee ambayo unaweza kujifunza na kupata historia mbalimbali za nchi hii. Na haya ni miongoni mwa matokeo bora y utunzaji na uhifadhi wa kumbukumbu kwa ajili ya kizazi kilichopo na kinachokuja.