Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Makumbusho ya Taifa la Tanzania

WASANII WATAKIWA KULETA MAONESHO YA KAZI ZA SANAA MAKUMBUSHO

Imewekwa: 11 Jan, 2024
WASANII WATAKIWA KULETA MAONESHO YA KAZI ZA SANAA MAKUMBUSHO

UNDAREY Art Gallery wamekabidhi picha ijulikanayo kama THE GREEN CITY kwa Mkurugenzi wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni, Bi. Adelaide Sallema wakati wa kufunga onesho la THE HEART MADE OF STONE lililofanyika kuanzia tarehe 25 Novemba mpaka tarehe 21 Disemba 2023 katika kituo Cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni jijini Dar es salaam.
Akizungumza baada ya tukio hilo Mkurugenzi wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni,
Bi.Adelaide Sallema amewashukuru UNDAREY GALLERY kwa kuleta onesho lao kwenye Makumbusho huku akitoa wito kwa wasanii wengine kuleta kazi zao ili zipewe nafasi ya kuonekana na kuwafikia watu wengi zaidi kwa haraka.
"Ninawashukuru sana Undarey Art Gallery kwa kushirikiana na Makumbusho, Msanii ametumia vitu ambavyo tunakutana navyo kila mara, ametumia taswira ya mawe kuonesha uhusiano baina ya binadamu na mazingira" amesema Bi Sallema na kuongeza,
"Ninaomba isiwe mwisho wasanii wengine pia wanakaribishwa kufanya maonesho mbalimbali kwa kuwa Makumbusho ya Taifa ni eneo rafiki kwa kazi za sanaa zinazolenga kufikisha ujumbe kwa jamii inayotuzunguka"
Onesho hili lililofungwa leo ni mwendelezo wa Programu maalum ya Sanaa na wasanii ijulikanayo kama 'MUSEUM ART EXPLOSION'(MAE) inayofanyika kila Mwisho wa mwezi katika Kituo cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Posta jijini Dar es salaam.