MAKUMBUSHO, MALIKALE ZITUMIKE KIUCHUMI

Imewekwa: 28th March, 2019

Na Joyce Mkinga, Songea

Siku ya tarehe 27 Februari ya kila mwaka ni siku kubwa sana kwa watu wa Songea, Mkoani Ruvuma kwa sababu ndiyo siku ambayo wakoloni wa Kijerumani waliwanyonga hadi kufa machifu na askari walioshiriki vita vya Maji Maji ambavyo vilipiganwa kati ya mwaka 1905 - 1907.

Wazee wa Jadi, Chifu wa Kingoni, askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na viongozi wengine wa Serikali hujumuika pamoja eneo la Makumbusho ya Maji Maji lililoko mjini Songea kuwakumbuka mashujaa hao ambao hawakukubali kutawaliwa na wakoloni.

Siku hiyo huanza kwa maandamano mpaka eneo walililonyongewa mashujaa wa vita vya Maji Maji ambapo gwaride la maombolezo hufanyika na kuweka silaha za jadi katika mnara ambapo askari wa vita vya Maji Maji walinyongewa wanne wanne kwa zamu mfululizo kwa siku mbili.

Baada ya hapo maandamano hayo yanayoongozwa na wazee wa Kingoni waliovalia mashuka mekundu kuelekea eneo walipozikwa mashujaa hao umbali wa kama mita 300 ambapo kuna uwanja mkubwa uliozungukwa na sanamu za machifu hao.

Katikati ya uwanja huo kuna sanamu kubwa ya askari yaliyebeba silaha midhiri ya askari aliye vitani. Katika sanamu hiyo huzunguka maskari nadhifu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliovalia sare za jeshi za mabaka mabaka na kitambaa cheusi juu ya mikononi yao walio tayari kwa amri ya kiongozi wao. Kiongozi hutoa amri na wimbo wa heshima kwa mashujaa hupigwa huku watu wengine wote wakiwa wametulia kimya kwa mfano wa mtu anayenyolewa.

Baada ya wimbo huo mizinga miwili ya heshima hupigwa ambayo pamoja na kutangaziwa kuwa itakuwepo bado watu hushtuka sana na wengine hudondoka na kuzimia. Hakika kila mwanandamu aliyezaliwa na mwanamke anayapenda maisha yake!

Baada ya heshima za kijeshi ndipo viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mgeni rasmi hutajwa mmoja baada ya mwingine kwenda kuweka silaha za jadi katika mnara wa kumbukumbu ya mashujaa wa vita vya Maji Maji ambapo kuna sanamu ya askari aliyekamata silaha.

Mgeni rasmi huweka ngao na mkuki, Mstahi Meya huweka upinde na mshale, kiongozi wa JWTZ huweka sime, Chifu wa Kingoni huweka shoka na Mzee wa Mila huweka rungu.

Sala na maombezi kwa ajili ya mashujaa hao kutoka kwa viongozi mbali mbali wa dini hufanyika na mashada ya maua huwekwa katika kaburi la halaiki na viongozi mbalimbali waliohudhuria maadhimisho hayo. Ngoma za asili na risala mbalimbali hutolewa kwa ajili ya kuwakumbuka mashujaa hao.

Mtafiti wa Makabila Mbalimbali Nchini, Bw Omela Musa anasema chanzo cha vita vya Maji Maji ni uonezi wa Wajerumani ambapo wananchi walichapwa viboko na kufanyishwa kazi ngumu kwa manufaa ya wakoloni hao. Vile vile walipigana kupinga kukandamizwa na kulazimishwa na wakoloni wa Kijerumani namna ya kuishi, mazao ya kuzalisha na kuwatumikia wao.

Vita vya Maji Maji vilianzia maeneo ya Kilwa ambapo kulikuwa na mtu anaitwa Kinjekitile Ngwale ambaye aliwashawishi watu kupambana dhidi ya mtutu wa bunduki wa Wajerumani waliokuwa wakiitawala Tanganyika akiwaahidi kuwalinda kwa maji ya miujiza. Jina la vita hii limetokana na imani ya matumizi ya dawa iliyochanganywa na Maji, punje za mahindi na mtama zilizosadikiwa kuwa zitampa mpiganaji kinga ya kutodhurika kwa shambulio la risasi za majeshi ya Wajerumani.

Mzee Musa anasema kuwa Chifu wa Wagoni wakati huo aliyeitwa Nkosi Mputa Gama bin Gwazerapasi alipopata taarifa kuwa kuna maji ya miujiza huko Kilwa, aliwatuma watu wake kwenda kuyaleta. Maji hayo yalifikishwa kwenye Makao Makuu ya chifu eneo liitwalo Maposeni.

Mratibu wa Kamati ya Wazee wa Mkoa wa Ruvuma Mzee Kassimu Yasini anasema vita vya Maji Maji Mkoa wa Ruvuma vilianzia eneo la Maposeni katika Makao Makuu ya Chifu Mputa Gama tarehe 21/08/1905 baada ya Wajerumani kuchoma kibanda cha Chifu.

"Wazee wa Kingoni walikasirika sana baada ya kuona kibanda cha Chifu kumechomwa moto hivyo, kuamuru vita dhidi ya Wajerumani vianze.

Vita vilipiganwa kwa nguvu sana, wakati Wajerumani walitumia mtutu wa bunduki Wangoni walitumia silaha zao duni za mishale, mikuki, mapanga na marungu. Mzee Yasini anasema japokuwa walikuwa na silaha duni lakini wingi wao uliwasumbua Wajerumani ambao ilibidi waongeze nguvukazi ya kupambana na wangoni

Chifu Mputa Gama alikuwa na wasaidizi 12 walioitwa manduna na mmojawapo alikuwa Nduna Songea Mbano ambaye alisifika sana na kuaminiwa na chifu kutokana na uhodari wake katika vita. Huyu ndiye aliyewaongoza Wangoni katika vita hiyo. Vita hiyo ya Maji Maji ilipiganwa kwa muda wa miaka miwili kuanzia mwaka 1905 mpaka 1907 ambapo kutokana na silaha duni walizotumia babu zetu walishindwa vita.

Mzee Yasini anasema mwisho wa vita hivyo askari wote na machifu walioshiriki vita hivyo walihukumiwa kunyongwa hadi kufa na wajerumani ambapo jumla ya watu 66 walinyongwa katika mnara wa kunyongea na kuzikwa katika kaburi la pamoja lililopo katika Makumbusho ya Maji Maji mjini Songea.

"Nduna Songea Mbano aliyekuwa kiongozi wa vita hivyo aliuwawa kwa risasi na kukatwa kichwa ambacho kilichuliwa na Wajerumani, anasema Mzee Yasini.

Kumbukizi ya vita hii hufanyika kila mwaka tarehe 27 mwezi wa pili ambapo Makumbusho ya Taifa la Tanzania chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii inaratibu shughuli hiyo katika mji wa Songea, mkoani Ruvuma kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Sekretariet ya Mkoa wa Ruvuma

Mwaka huu wa 2019 ni maadhimisho ya 112 ambapo pamoja na mambo mengine mkazo kubwa umewekwa katika kukumbuka uthubutu wa mashujaa hao katika kutetea haki na uhuru wao.

Akisungumza katika hafla hiyo Katibu Mkuu wa Wizira ya Maliasili na Utalii, Prof Adolf Mkenda anasema kuwa maadhimisho ya Kumbukizi ya Vita vya Majimaji na Utalii wa Utamaduni kwa mwaka 2019 yanalenga katika kuenzi uthubutu wa mababu zetu waliopanda mbegu ya uzalendo, utaifa, amani, upendo na mshikamano wa Taifa letu.

"Kumbukizi hii hutoa fursa kwa wananchi kushiriki katika kutunza, kuenzi na kuendeleza uthubutu, uzalendo, amani na mshikamano, vitu ambavyo ni miongoni mwa urithi tuliorithi kutoka kwa mababu zetu na waasisi wa Taifa letu" Anasema Prof Mkenda katika hotuba ya Mahudhui ya maadhimisho hayo iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa wizara hiyo Bw. Liusius Mwenda.

Anasema siku hii pia hutumika kuibua na kuendeleza vivutio vya utalii vinavyopatikana katika Ukanda wa Kusini hususan Mkoani Ruvuma.

Tangu mwaka 2011 tamasha hili limeshirikisha wageni kutoka Malawi, Msumbiji na Zambia ambapo machifu wa makabila ya Wagoni waishio katika nchi hizo. Mwaka huu wa 2019 wageni watatu kutoka Malawi walijumuika pamoja na wenzao katika kumbukizi hiyo.

"Lengo kuu ni kutumia utalii wa malikale katika kuimarisha urafiki na ujirani mwema baina ya nchi yetu na mataifa mengine" anasema Prof Mkenda.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Prof. Audax Mabulla anasema lengo la Serikali kuendelea kuyatunza maeneo ya malikale ni kuhakikisha kuwa maeneo hayo yanatumika kiuchumi na kitaulii badala ya kihistoria pekee.

"Hatuna vita vya wakoloni tena hivyo, vita vyetu viwe vya kujikomboa kiuchumi, anaseama Prof Mabula.

Prof Mabula anasema kuwa ushahidi maridhawa kuwa binadamu wa kwanza duniani aliishi Tanzania ni eneo la Olduvai Gorge ambako kuna mabaki ya mwanadamu wa kwanza. Eneo hili licha ya kuwa ni muhimu kwa historia ya nchi yetu ni kivutio cha utalii kwa wageni na wazawa.

" Tunatakiwa kuangalia ni kwa namna gani maeneo haya yanaweza kutumika kiutalii hivyo kunufaika kiuchumi," anasema Prof. Mabula.

Anatoa wito kwa wananchi kutemebelea maeneo ya makumbusho kwa sababu ni tunu za nchi yetu na maeneo muhimu kwa elimu na utafiti.

Mgeni Rasmi katika kumbukizi ya Mashujaa wa vita vya Maji Maji mwaka huu 2019 alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Bibi Christina Solomoni Mndeme ambaye alielezea uthubutu wa mashujaa hao katika kutetea nchi yetu na kwamba unafanana kabisa na uthubutu alionao Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John Pombe Magufuli katika kujenga uchumi wa Tanzania.

"Njia nzuri ya kuendelea kuwaenzi mashujaa hawa ni kuunga mkono na kutekeleza kwa vitendo dhana ya hapa kazi tu ya Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzanania anayoitumia kuhimiza kila Mtanzania kufanyakazi kwa bidii, kulinda rasilimali za taifa, kupambana na kuzuia rushwa na madawa ya kulevya" anasema Bibi Mndeme

Anasema Sera ya Malikale inatoa ruhusu kwa sekta binafsi kushiriki katika kuyamiliki, kuyaendeleza, kuyahifadhi na kuyatumia kama chanzo cha uchumi maeneo ya makumbusho kama haya ya Vita vya Maji Maji na mengineyo.

"Natoa wito kwa Watanzania wote kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kuyaendeleza na kuyahifadhi maeneo haya ili kiwe chanzo cha ajira kwa wananchi wote" Anasema Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.

Maeneo haya yanaweza kuchangia katika kupambana na umaskini kama vile ambavyo yalichangia katika mapambano dhidi ya unyanyasaji wa kikoloni.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma analipongeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kushiriki kikamilifu katika kumbukizi ya 112 ya Mashujaa wa Vita vya Maji Maji ambapo lilifanya gwaride la heshima na kupiga mizinga ya heshima kwa mashujaa hao.

Mwisho