MAENDELEO YASIHARIBU URITHI WA ASILI

Imewekwa: 03rd March, 2020

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Aloyce Nzuki amesema maendeleo yoyote yanayofanyika maeneo mbalimbali nchini yaangalie umuhimu wa kutunza historia na utamaduni wa Mtanzana.

Dkt. Nzuki ameyasema hayo mwishoni mwa wiki alipotembelea eneo la Maposeni Peramiho mahali ambapo vita vya Maji Maji vilianzia.

Amesema kuwa kwa kadri nchi inavyotaka maendeleo kuna hatari ya kupoteza historia na utamaduni wa nchi, hivyo ni muhimu jambo hili likatazamwa na wahusika mbalimbali.

Dkt. Nzuki ambaye aliongozana na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Noel Lwoga amesema Serikali za Mitaa na Serikali kuu pamoja na wadau wengine katika jamii ni lazima wafanye kazi kwa pamoja ili kuokoa urithi wa asili wa Mtanzania.

“Maendeleo tunayataka na urithi wa asili lazima huifadhiwe kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho,” amesema Dkt. Nzuki.

Dkt Nzuki na Dkt Lwoga walikutana na Chifu wa Wangoni Inkosi Emmanuel Zulu Gama na wasaidizi wake pamoja na Chifu wa Malawi Inkosi ya Makhosi Mmbelwa wa Tano ambao wote walitembelea eneo la Maposeni kama sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 113 ya Vita vya Maji Maji.

Pamoja na mambo mengine walitembelea kaburi la Father Francis ambaye aliuwawa na Wangoni baada ya kuchoma kibanda cha chifu wa Wangoni walichokuwa wanakitumia kwa ibada za kimila.

Kwa picha, https://www.nmt.go.tz/galleries