DKT LWOGA: WATAALAMU ANDIKENI MIRADI YA KULISAIDIA TAIFA, KUHIFADHI NA KUENDELEZA URITHI WETU

Imewekwa: 30th April, 2020

Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt Noel Lwoga amewataka wataalamu wa Tasisi hiyo kuongeza umakini na ubunifu katika kuandika miradi mbalimbali inayo endana na shughuli za msingi za makumbusho.

Dkt Lwoga ametoa wito huo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizindua rasmi utaratibu wa kuwasilisha andiko la miradi katika jopo la wataalamu wa Miradi wa Taasisi hiyo kwa ajili ya kujadiliwa na kufanyiwa maboresho.

Amesema watalaamu hao wanatakiwa kuandika miradi inayoendana na kazi za Makumbusho ya Taifa ambazo ni pamoja na kuhifadhi urithi wa asili na utamaduni wa nchi na kutoa elimu kwa wananchi wa Tanzania.

"Nawapongeze wote mliwasilisha maandiko yenu ya miradi leo, hii inatupa picha halisi ya namna mlivyo na mawazo mazuri yatakayowezesha Taasisi yetu kuimarika katika uhifadhi wa urithi wa asili na utamaduni,” amesema Dkt Lwoga.

Dkt. Lwoga amesema kuwa katika maandika hayo ya miradi wapo wadau wengi watakaounga mkono katika utekelezaji wake kwa sababu ni muhimu na ni kwa maslahi mapana ya Taifa letu.

Awali akimkaribisha Mkurugenzi Mkuu wa Makumbisho ya Taifa, Mkuu wa Idara ya Mipango na Ufuatiliaji wa Makumbausho ya Taifa, Bw Mawazo Ramadhani alisema kuwa utaratibu huu ni mpya ambao unalenga katika kuinua vipaji vya uandishi wa miradi.

Bw Ramadhani amesema utaratibu huu utaibua miradi mikubwa ambayo itasaidia Taasisi kuongeza mapato na kuendeleza uhifadhi endelevu wa mikusanyo ya kimakumbusho.

Naye Mkurugenzi wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni, Bw Achiles Bufure aliupongeza uongozi wa juu wa Makumbusho ya Taifa kwa kuanzisha utaratubu huo na kwamba utaibua miradi mingi.

“Utaratibu huu ni ukombozi kwetu maana utaibua miradi mingi hususan katika kituo chetu,” alisema Bw. Bufure.

Miradi iliyowasilishwa ni pamoja na Uhifadhi wa Urithi wa Rasilimali Madini, na Mapambano dhidi ya Mimba za Utotoni kupitia Sanaa na Wasanii, kutoka kituo cha Makumbusho na Nyumba ya Utamadhuni na Uboreshaji wa Kijiji cha Makumbusho (Mradi wa Kijiji cha Makumbusho)