Sanaa

Maonyesho ya Sanaa ni Miongoni mwa kumbi zinazopatikana Makumbusho ya Taifa. Maonyesho haya yalifunguliwa kwa lengo la kuonyesha kazi mbalimbali za sanaa za wasanii kutoka Tanzania, kwa lengo la kuiwezesha jamii iweze kujifunza, kuelewa na kutambua umuhimu wa kazi za sanaa kupitia michoro pamoja na michongo mbalimbali ya vinyago vya kimakonde.

Kumbi hizi zina kazi za wasanii kuanzia miaka ya 1970's akiwemo Profesa Sam Joseph Ntiro na Profesa Elius Jengo kutoka chuo Kikuu cha Dar es salaam. Pia Jamii inajifunza mengi kutoka kwenye michoro ya Tingatinga kutoka kwa msanii mashuhuri Edward Said Tingatinga, na wasanii wengine kama vile Doreen Mandawa, Raza Mohamed, Muzu Selemanji, Robino Ntila na L.M. Patel katika kazi zao za sanaa za kisasa.

Michongo ya vinyago vya kimakonde kutoka kwa wasanii kama Kashmir Mathayo na Petro Paul Magiye vinasaidia kuelimisha jamii na hii ni kutokana na michongo hii kupatikana katika jamii na kuonyesha sura mbalimbali na mabadiliko yanayojitokeza. Vilevile mbali na kupatikana kwa michoro na michongo mbalimbali katika kumbi za sanaa pia kuna michoro ya miambani na michongo ambayo iliweza kutumiwa na jamii ya wakulima na wafugaji miaka mingi iliyopita. Waliweza kutumia kama chombo cha mawasiliano na pia kukabiliana na matatizo mbalimbali waliyokuwanayo kama vile kujitibia katika magonjwa mbalimbali, kutoa kafara, kufanyia ibada n.k

Pia kuna sanaa za nje ikiwemo Maonyesho ya mabaki ya nyumba ya sanaa ya George Lilanga mmoja wa wasanii wa kwanza Tanzania aliyejulikana ulimwengu mzima kwa michoro yake ya shetani na roho chafu ambazo makazi yake ni kwenye ulimwengu halisi na ulimwengu wa kiroho. Lilanga ilikuwa ni sehemu ya nyumba ya sanaa (1972-2012) Ambayo iliibua vipaji vya wasanii mbalimbali akiwemo Robino Ntila, Augustino Malaba, Walter Lemaponi yengi na wengineo.

Pia unaweza kuona kazi ya sanaa iliyotengenezwa kwa kutumia miti ya mininda ambayo inaonyesho mfano wa nyumba zilizokuwa zikijengwa na wakazi wa Dar es Salaam kabla ya kuendelea kwa Teknolojia ya ujenzi wa kisasa wa kutumia vioo, sanasana watu wa tabaka la chini pamoja na wafanyakazi.

Hivyo basi kumbi za sanaa zinatoa fursa kwa wageni na wenyeji kuja kutembelea ili kujionea, kujifunza, na kufurahia sanaa mbalimbali za Tanzania ikiwa ni moja ya nyenzo za kutunza, kuhifadhi, kuthamini na kutangaza utamaduni wetu ndani na nje ya Tanzania