NMT NA TAKA YANGU HAZINA YANGU YAINGIA JIJINI MBEYA

Imewekwa: 12th August, 2019

Na Bi Joyce Mkinga


AFISA Mazingira wa Jiji la Mbeya, Bw. January Nduguru amewataka wananchi wa mkoa huo kutumia taka kama malighafi ya kutengenezea vitu vinavyoweza kuwaletea kipato badala ya kuzitelekeza mitaani.


Bw. Ndunguru amesema elimu ya kutumia takataka kutengeneza vitu na kutenganisha takataka kulingana na makundi yake (taka ngumu, mabaki ya vyakula na taka hatarishi) ni muhimu kwa wananchi wa mkoa wa Mbeya kwa sababu itaokoa mazingira na kuwaongezea kipato.


Afisa Mazingira wa Jiji la Mbeya ameyasema haya hivi karibuni katika onesho la sanaa la Taka Yangu, Hazina Yangu lilioandaliwa na taasisi ya Makumbusho ya Taifa kwa kushirikiana na wasanii wa sanaa za ufundi na jukwaani wa mkoa wa Mbeya.


Katika Onesho hilo wasanii wa sanaa za ufundi walionesha vitu mbalimbali vilivyotengenezwa kwa kutumia taka ambazo walizibadilisha na kutengeneza vitu mbalimbali vya kutumika majumbani.


Vitu hivyo ni pamoja na mito ya kulalia iliyotengenewa kwa kutumia nywele na mawigi yanayotupwa kwa wasusi na vinyoozi, mkaa uliotengenezwa kwa kutumia karatasi, mabango ya urembo yaliyotengenezwa kwa kutumia majani ya migomba ya ndizi na vitu vingine vilivyotengenezwa kwa chupa za glasi na plastiki.


Pamoja na onesho la sanaa za ufundi kulikuwa na sanaa za jukwaani ambapo wasanii walionesha maigizo, ngoma, muziki na mazingaombwe yenye maudhui ya kuelimisha jamii kuhusu kutumia takataka kutengeneza vitu vingine.


Bwana Ndunguru amesema kuwa kama wananchi wote wa mkoa wa Mbeya wataitikia na kutumia elimu hii kikamilifu itaokoa fedha nyingi zinazotumika katika kuzoa na kuchakata takataka katika dampo la isalanga


“Wananchi wote wakifuata na kutekeleza elimu hii itasaidia kupunguza uzalishaji wa takataka zinazotupwa kataka dampo letu na hivyo kulifanya likae muda mrefu.


Amesema jiji la Mbeya linazalisha zaidi ya tani 230 kwa siku na uwezo wa jiji ni kuzoa tani 165 tu. Amesema wanakusanya taka zinazooza asilimia 77, plastiki (5) nguo (4) pumba (3), vioo (2), mbao (4) na zinginezo (3).


Afisa Mazingira amesema elimu hiyo itaendelea kutolewa kwa wananchi wote wa mkoa wa Mbeya mijini na vijijini ili kuokoa mazingira na pia kuwaongezea kipato wananchi kwa sababu vitu vinavyotengenezwa vinauzwa na vinanunuliwa sana.

Makumbusho ya Taifa kwa kushirikia na Jiji la Mbeya pamoja na wasanii wa sanaa za ufundi na jukwaani wa mkoa wa Mbeya walifanya maonesho shirikishi ya kuelimisha wananchi saba katika maeneo ya kituo cha mabasi cha Kabwa na Nanenane, Shule ya Sekondari Mbeya na Lyoto, Shule za msingi za Mbata, Majengo, Kagerea na Ruanda Nsove.


Awali Mkuu wa Idara ya Programu wa Makumbusho ya Taifa, Bw. Chance Ezekiel alisema kuwa wananchi wanatakiwa kuelimishwa juu ya kutenganisha takataka kulingana na makundi yake ili iwe rahisi kwa wasanii wanaotengeneza vitu mbalimbali kuzinunua kwa ajili ya kutengenezea vitu mbalimbali.


“Kama hizo takataka zimechanganywa inakuwa vigumu mtu kununua kwa ajili ya kutengenezea vitu mbalimbali” alisema Bw. Ezekiel.


Makumbusho ya Taifa la Tanzania kupitia programu yake ya Sanaa na Wasanii ijulikanayo kama Museum Art Explosion inatekeleza mradi wa Taka Yangu Hazina Yangu (My Trash My Treasure).


Mradi huu unalenga katika kuelimisha umma juu ya matumizi ya takataka kama malighafi ya kutengenezea vitu mbalimbali ambavyo vinaweza kutumika katika jamii.


Mradi huu unatumia sanaa za jukwaani na za ufundi katika kutoa elimu kwa wananchi ambapo unaangalia ni kwa namna gani mtu anaweza akafaidika na takataka kwa kuzirejerea (recycling).


Mradi pia unatoa elimu ya kupanga (sorting) kulingana na aina ya takataka kwa mfano karatasi, plastic, vitambaa, mabaki ya vyakula na kadhalika.


Mradi huu utatekelezwa katika mikoa ya Dodoma, Mbeya na Dar es Salaam ambapo wasanii wa mkoa husika wanatumika katika kutoa elimu ya matumii ya taka katika kutengeneza vitu vinayoweza kutumika tena katika jamii kwenye mikoa yao.,


Katika utekelezaji wa mradi huu Makumbusho ya Taifa la Tanzania inashirikiana na Ubalozi wa Uswiss nchini Tanzania katika kuhakikisha kwamba elimu hii inawafikia wananchi.


MWISHO