MAKUMBUSHO YA TAIFA YAMUENZI MSANII MAARUFU BIBI DOREEN MANDAWA

Imewekwa: 01st November, 2019

Makumbusho ya Taifa imemuenzi Msanii maarufu nchini Bibi Doreen Mandawa kwa kuweka onesho maalum la picha zilizochorwa na Msanii huyo nguli ili kutoa nafasi kwa watanzania na wageni wa kimataifa kujifunza urithi wa Kihistoria na wa kimazingira kupitia kazi hizo za Sanaa.

Akifungua onesho hilo maalumu, Balozi wa Norway nchini Mhe. Elizabeth Jacobse ameipongeza Makumbusho ya Taifa kwa kazi nzuri ya uhifadhi wa Urithi wa Utamaduni kupitia kazi za wasanii mbali mbali hasa za Bibi Doreen Mandawa kwa kuandaa program za maonesho ya kazi hizo.

Sanaa ina mchango mkubwa katika kuelimisha na kuibadilisha jamii kifikra na ujumbe huo ukaishi kwa muda mrefu sana katika akili za watu hivyo nimefurahi kuwa sehemu ya sherehe ya kuenzi kazi za sanaa na mchango wake katika jamii” Alisema Balozi Jacobse.

Akizungumza kwa niaba ya Marafiki wa Bibi Mandawa waishio Norway Balozi mstaafu Norway nchini Mhe Dag Nissen amemuelezea Msanii huyo Mkongwe kuwa, amekuwa akifanya kazi zake zenye kuangazia changamoto za kijamii, mafanikio na uzuri wa mazingira ili kufikisha ujumbe kwa jamii, kilichopelekea watu wengi kuvutiwa na kazi zake.

Kutokana na Mchango wake mkubwa alioutoa nchi mbali mbali hasa Norway kwa kufanya maonesho yaliyovutia wengi na kuwafanya watu wanunue michoro yake, tukaona ni vyema tuje Tanzania sehemu alieamua kuishi ili tusherekee nae miaka 90 ya kuzaliwa kwake.” Aliongeza Balozi Mstaafu Nissen.

Nae Prof Anna Tibaijuka akiwa miongoni wa watu walioudhuria sherehe za kuzaliwa Bibi Doreen Mandawa na ufunguzi wa onesho hilo maalum, alisema kuwa amemfahamu Msanii huyo kupitia Balozi Nissen ndipo akaaza kumfuatilia kupitia kazi zake za Sanaa zinazoonesha namnaa alivyojitoa kuelimisha jamii hivyo Makumbusho ya Taifa imefanya vyema kumuheshimu na kuenzi.

Msanii Mkongwe nchini Prof Elias Jengo ambae ni mmoja wa wasanii waliofanya kazi kwa ukaribu na Bibi Mandawa, alimuelezea Msanii huyo kuwa mbunifu ambaye hanakili vitu bali anatafsiri vitu na kuweka katika Sanaa yake ya uchoraji na hata hivyo amesaidia kuleta mwamko kwa wasanii wachanga ambao kwa sasa wengi wao wamekuwa wasanii wakubwa nchini.

Akiwa na nyusa ya furaha, Msanii Doreen ameishukuru Makumbusho ya Taifa pamoja na Marafiki zake, kwa zawadi kubwa waliyompatia ya kusherekea siku yake ya kuzaliwa kwa njia ya kuenzi kazi zake na kumkutanisha na marafiki aliopotezana nao kwa miaka mingi.

Licha ya kuwashukuru wote walioa udhuria sherehe hiyo, kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Mkurugenzi wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Bw Achiles Bufure, amewashukuru marafiki wa Bibi Doreen Mandawa kutoka Norway kwa kushirikiana na Makumbusho ya Taifa kuandaa onesho hilo, pia amemshukuru Balozi wa Norway nchini Mhe Elizabeth Jacobse kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika sherehe hiyo, na ameahidi kuwa Makumbusho ya Taifa itaendelea kuthamini, Kuhifadhi na kuenzi kazi za wasanii nchini.

Msanii Bibi Doreen Mandawa ambaye tarehe 30 Oktoba 2019 ametimiza miaka 90, asili yake ni Uingereza (Scotish) amekaa Tanzania zaidi ya miaka 50 baada ya kuolewa na Mtanzania Marehemu Mzee Mandawa na onesho lenye kazi zake za Sanaa litakuwepo kwa Muda wa mwezi mzima katika ukumbi wa King George uliopo Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar es Salaam.

https://www.nmt.go.tz/galleries