KUMUENZI MWALIMU NYERERE MIAKA 20 YA KIFO CHAKE

Imewekwa: 21st October, 2019

Ubalozi wa Marekani chini Tanzania umetoa picha za ziara za kihistoria za Mwalimu Nyerere nchini Marekani kwa Makumbusho ya Taifa.

Picha hizo zimekabidhiwa kwa Makumbusho ya Taifa jana na Afisa wa Ubalozi anayeshughulikia Maswala ya Umma, Bibi Brinille Ellis.

Picha hizi ambazo ni tangu miaka ya 1960 zinaonesha jinsi Tanzania ambavyo imekuwa ikishirikiana na nchi ya Marekani.

Afisa anayeshughulikia Masuala ya Umma wa Ubalozi wa Marekani amesema kuwa picha hizo zimekabidhiwa kwa Makumbusho ya Taifa kama sehemu ya kumuenzi Mwalimu Nyerere wakati wa kumbukumbu ya kifo chake miaka 20 iliyopita.

Bibi Ellis amesema vile vile msaada wa picha hizo zilizo katika ubora wa hali ya juu unalenga katika kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya Tanzania na Marekani.

“Tunatoa picha hizi kwa ajili ya kumuenzi Mwalimu Nyerere na kwa ustawi wa ushirikiani wetu na Tanzania,” amesema bibi Ellis.

Amesema kuwa jozi ya picha zilizotolewa katika Makumbusho ya Taifa Dar es Salaam itatolewa pia katika Makumbusho ya Mwalimu Nyerere iliyoko katika Kijiji cha Mwitongo, Butiama

Moja ya picha hizo inawaonesha Rais wa zamani wa Marekani Mhe. Kennedy wa Marekani na Waziri Mkuu wa Tanganyika, Julius Kambarage Nyerere katika Ikulu ya White House jijini Washington DC tarehe 17 Septemba mwaka 1961.

Picha nyingine inamuonesha kiongozi wa harakati za kupigania haki za raia, Dkt, Martin Luther King Jr, akizungumza na Rais wa Tanganyika Julius Kambarage Nyerere katika dhifa iliyoandaliwa na Rais Kenndy huko Washington DC tarehe 16 Julai 1963.

Picha nyingine ya miaka ya karibuni ni ile inayomwonesha Rais Mstaafu wa Marekani Jimmy Carter akimkaribisha Rais Mstaafu wa Tanzania, Mwalimu Julius K. Nyerere, Atlanta, Georgia, Marekani tarehe 8 Mei 1998 mwaka mmoja kabla ya kifo chake.

Akizungumza wakati wa kupokea picha hizo jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Gwakisa Kamatula ameshukuru Ubalozi wa Marekani kwa picha hizo ambazo zitaongeza ufanisi wa maonesho yanayomhusu Mwalimu Nyerere katika Makumbusho hiyo.

“Tunawashukuru wenzetu wa Marekani kwa mchango wa picha hizi maana zimekuja katika wakati muafaka tunapokumbuka miaka 20 tangu kifo cha Mwalimu Nyerere,” amesema Dkt. Kamatula.

Dkt. Kamatula amesema kuwa msaada huu unaonesha jinsi Mwalimu alivyoweka msingi mzuri wa mashirikiano kati ya nchi yetu na mataifa mbalimbali duniani