UKATAJI MITI OVYO WACHOCHEA UPUNGUFU WA VIPEPEO, NONDO WAZALISHAO MAZAO

Imewekwa: 21st October, 2019

Mahitaji makubwa ya ardhi, mabadiliko ya tabia nchi na uchafuzi wa mzingire ni miongoni mwa sababu zinazosababisha kupungua kwa vipepeo na nondo wachavushao katika ukanda wa Afika Masharika.

Kulingana na tafiti zilizofanyika katika Milima ya Usambara hususan Hifadhi ya Misitu ya Amanii Mkoa wa Tanga Novemba 2017 mpaka Juni 2019 kumekuwa na mabadiliko ya wingi wa vipepeo na nondo na idadi kubwa ya aina za vipepeo inapungua.

Mmoja wa watafiti wa Tathmini ya Mtawanyiko wa Taarifa za Vipepeo na Nondo Afrika Mashariki, Bibi Adelaide Sallema anasema jumla ya tafiti tatu zilifanyika ambapo waligundua kuwa kumekuwa na mabadiko ya wingi na aina ya vipepeo wachafishao katika milima hiyo ambapo wamekuwa wakipungua kwa kasi

Akizungumza katika mkutano wa kutoa taarifa za utafiti uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Bibi Sallema anasema Mifumo ikolojia mingi Afrika Mashariki inakabiliwa na tishio la mabadiliko ya matumizi na ongezeko la uhitaji mkubwa wa ardhi kwa ajili ya kilimo, uchafunzi wa mazingira, uingizaji wa aina ngeni za vipepeo na mabadiliko ya tabia nchi.

“Kumekuwa na ongezeko kubwa la ukataji miti kwa ajili ya mashamba ya kilimo tofauti na siku za nyumba jambo ambalo linahatarisha uwepo wa wadudu wachavushao kama vipepeo na nondo” anasema Bibi Sallema.

Bibi Sallema ambaye ni Mtaalam wa Biolojia kutoka Makumbusho ya Taifa la Tanzania anasema kuwa kumekuwepo na changamoto ya uelewa mdogo wa vipepeo na nondo kama viumbe wachavushao miongoni mwa wananchi.

Kulingana na tafiti zilizofanyika katika Hifadhi ya Misitu ya Amani vipepeo na nondo ni wadudu wachavushaji wakuu wa mazao ya misitu ya asili na mashamba yaliyo pembezoni mwa hifadhi hiyo lakini kutokana na uelewa mdogo wanaonekana kama ni wadudu waharibifu mashambani.

“Vipepeo na nondo ni wadudu muhimu katika uzalishaji wa mazao kwa sababu husaidia katika uzalishaji wa mazao hivyo ni vema wakahifadhiwa” anasema Bibi Sallema.

Vipepeo na nondo wanachangia upatikanaji wa chakula na kusaidia kazi za mfumo wa ikolojia, lakini wamekuwa wanaathirika na ukataji wa miti na mimea waipendayo.

Anaeleza kuwa utafiti ulifanyika kwa kutumia dodozo kutambua watumiaji wa taarifa za bionuai katika taasisi sita. Matokeo yanaonesha kuwa asilimia 89 ya wadau wanahitaji taarifa za bianuai kutoka katika taasisi sita zilizohojiwa. Hata hivyo ni asilimia 32 tu wanaohitaji taarifa za vipepeo na nondo ukilinganisha na asilimia 54 wanaohitaji taarifa za mimea.

Watafiti waligundua kuwa taarifa za vipepeo na nondo ni chache kwa taasisi nyingi Serikalini, hivyo ni vigumu kukabiliana na uhitaji wa sasa wa mazao kupitia huduma ya uchavushaji, anasema Bibi Sallema na kuongeza kuwa hii inaonyesha kuwa kuna uhaba wa elimu kuhusu vipepeo na nondo kama wadudu wachavushao.

Katika kupambana na changamoto hiyo mradi wa pamoja wa miaka mitatu (2017 – 2019) ujulikanao kama Tathimin ya Mtawanyiko wa Taarifa za Aina za Vipepeo na Nondo Afrika Mashariki umekuwa ukitekelezwa na nchi tatu za Tanzania, Uganda na Kenya.

Mratibu wa Mradi huo unaotekelezwa na Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Makumbusho ya Taifa la Kenya na Makumbusho ya Zoolojia katika Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda, Dkt. Ester Kioko anasema mradi unalenga katika kutathmini wingi wa idadi ya vipepeo na nondo na aina za mimea inayohusiana katika Hifadihi ya Milima ya Misitu ya Amani hususan Milima ya Usambara Mashariki ambako kunasadikika kuwa na vipepeo wengi.

Dkt. Kioko ambaye ni Mkuu wa Idara ya Zoolojia, Makumbusho ya Taifa Kenya

anasema kuwa mradi vile vile unalenga katika kujenga uwezo katika nyanja za ukusanyaji, utambuzi, usajili, utengenezaji ramani, uandaaji machapisho na ushirikishaji taarifa zinazohusiana na vipepeo na nondo.

Mradi umefanya program za uhamasishaji jamii kuhusu umuhimu wa wadudu wachavushao katika mazingirea, hivyo mradi umejenga uwezo wa utunzaji wa taarifa za viumbe wachavusaho katika maeneo ambapo utafiti umefanyika.

“Ushirikishaji na uhamasishaji ni muhimu kwa sababu maoni ya jamii yanaweza kusaidia katika kutunga sera na sheria mbalimbali kupitia tafiti na taarifa sahihi kwa ajili ya maamuzi,” anasema Dkt. Kioko.